-Aeleza matarajio ya Serikali ya awamu ya sita ni kuona miradi  ya kimkakati ukiwemo  hoteli ya nyota tano jijini Mwanza unakamilika
 
Na MWANDISHI WETU,
 
Mwanza. Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhe. Said Mtanda amesema ni azma ya Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuona miradi ya kimkakati ukiwemo hoteli ya nyota tano inayojengwa na Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) jijini Mwanza inakamilika.

Mhe. Mtanda amesema hayo mwishoni mwa wiki wakati alipofanya ziara ya kikazi kukagua miradi ya kimkakati.

“Nawapongeza NSSF kwa kazi nzuri na ubunifu mkubwa wa miradi ya kimkakati wanayoitekeleza sehemu mbalimbali nchini, nawaomba waendelee kuongeza  kasi ya utekelezaji ili ile azma ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kuona miradi mbalimbali ya kimkakati inakamilika kama ilivyokusudiwa.

Mhe.Mtanda amesema mradi  wa NSSF wa hoteli ya nyota tano wa jijini Mwanza, utakapokamilika utaongeza thamani katika jiji hilo, amewahakikishia  Serikali ya Mkoa  itaendelea kutoa ushirikiano kwa NSSF kuhakikisha mradi huo unakamilika na kuanza kutumika kama ilivyokusudiwa.

Awali, akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Kaimu Mkurugenzi wa Uwekezaji, Bw. Mapesi Maagi amesema uwekezaji wa mradi huo ni moja kati ya majukumu manne ya Mfuko ambayo ni kuandikisha wanachama kutoka sekta binafsi na sekta isiyo rasmi, kukusanya michango, kuwekeza na kulipa mafao. 

Bw. Maagi amesema uwekezaji wa hoteli hiyo utakapokamilika utachochea maendeleo ya Mkoa wa Mwanza na Kanda ya Ziwa kwa ujumla kwa kuinua shughuli za kiuchumi hususan utalii hasa ukizingatia kuwa Mkoa wa Mwanza umepakana na Hifadhi ya Taifa ya Serengeti ambayo ipo karibu na mkoa huo.

Naye, Meneja wa NSSF Mkoa wa Mwanza, Bw. Emmanuel Kahensa amemshukuru Mkuu wa Mkoa kwa kufanya  ziara hiyo ya kikazi katika mradi huo wa hoteli ya nyota tano.

Akitoa taarifa, Mhandisi Helmes Pantaleo ambaye ni Meneja Miradi wa NSSF ameelezea utekelezaji wa mradi  na changamoto zote ambazo zilikuwa ni kikwazo zimetatuliwa. Mhandisi Pantaleo amesema utekelezaji unaendelea ambapo unatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwaka huu na kuanza kazi mwezi Machi 2025.


Na Mwandishi Wetu

Dar es Salaam. Kampuni ya michezo yakubashiri ya Parimatch imezindua michuano maalum ijulikanayo kwa jina la Parimatch Kitaa Cup 2024 yenye lengo la kuinua na kundeleza vipaji katika mpira wa miguu.

Mashindano haya yanashirikisha jumla ya timu nane kutoka maeneo mbalimbali ya jijini Dar es Salaam kwa mujibu wa Mkuu wa Masoko wa kampuni hiyo, Levis Paul.

Paul alizitaja timu hizo kuwa ni Faru Dume, Karume FC, Kawe UTD, Makubuli FC, Kauzu FC, Namanga FC, Mpakani FC pamoja na Rangi tatu FC.

Katika mchezo wa ufunguzi, Faru Dume iliifunga timu ya katume United kwa mabao 2-0 wakati Kawe United iliichapa Makubuli kwa bao 1-0 na Kauzu ikiifungashia virago Namanga kwa mabao 2-0 kutinga nusu fainali ambayo itachezwa leo Jumapili kwenye viwanja hivyo hivyo.

Mshindi wa mashindano hayo ya siku mbili atazwadiwa sh1milioni na wa pili atapata sh500, 000. Pia kutakuwa na zawadi ya mshindi wa tatu ambayo ni mipira miwili katika mashindano hayo ya
Kwa mujibu wa Paul, pia kutakuwa na zawadi ya mfungaji bora, golikipa bora pamoja na mchezaji bora wa kila mchezo.

"Timu zote shiriki zimepewa jezi na mpira ambazo zinatumika katika mashindano na morali ya kila mchezaji ipo juu," alisema Paul.

Alisema kuwa kampuni ya Parimatch imedhamiria kuchangia maendeleo ya michezo nchini kwa vitendo na hasa kwa timu za mitaani ambapo kuna wachezaji wengi wanaoweza kuleta mafanikio kwa klabu mbalimbali na timu ya Taifa.

"Kutokana na hilo, ndiyo maana tumeandaa mashindano haya ya muda mfupi, kusaidia vifaa vya michezo na kuweka zawadi nono, hii itasaidia wachezaji kupambania timu zao ili kuibuka washindi.
Nawaomba mashabiki wa soka wa Dar es Salaam kujitokeza kwa wingi ili kupata burudani safi kutoka timu zetu za mitaani, "alisema.

Kampuni ya Parimatch ni kinara wa michezo ya kubashiri mtandaoni na imekuwa ikitoa ofa kubwa ya bonasi ya ukaribisho ya asilimia 125 hadi kufikia Sh 1,000,000 kwa wateja wapya wanaojiunga nao.

Parimatch imekuwa ikifanya kazi nchini Tanzania tangu mwaka 2019, ikitoa huduma nzuri ikijumuisha malipo ya haraka, odds kubwa na promosheni za kusisimua kwenye soka, Kasino na Michezo ya virtual. Mbali na soka, kampuni ya Parimatch pia hutoa mamia ya matukio kila siku kwenye tenisi, UFC, mpira wa vikapu, Kriketi, baseball na michezo mingine mingi ya Live na pre-match.
 

Wachezaji wa Faru Dume na Karume United wakichuano katika mechi ya ufunguzi ya Parimatch Kitaa Cu 2024 kwenye uwanja wa Zakhiem, Mbagala jijini Dar es Salaam.

 

Mwenyekiti wa Chama Cha soka cha Manispaa ya Temeke (TEFA), Ally Kamtande na Mkuu wa Masoko wa kampuni ya michezo ya kubashiri ya Parimatch, Levis Paul wakikagua timu ya Karume United kabla ya kuanza kwa mchezo wa ufunguzi wa mashindano ya Parimatch Kitaa Cupn2024 kwenye uwanja wa Zakhiem, Mbagala.

 

Wachezaji wa Faru Dume na Karume United wakichuana wakati wa ufunguzi wa mashindano ya Parimatch Kitaa Cup 2024 kwenye uwanja wa Zakhiem, Mbagala.

 

Wachezaji wa timu ya Faru Dume FC wakiwa katika picha ya pamoja kabla ya kuanza kushiriki mashindano ya Parimatch Kitaa Cup 2024 kwenye uwanja wa Zakhiem, Mbagala jijini Dar es Salaam.

DODOMA: Kamishna wa Madini Dk Abdulrahman Mwanga ameongoza kikao kazi cha wataalam wa Wizara, Tume ya Madini na wawakilishi wa Umoja Wafanyabiashara wa Baruti Tanzania (TEDA) kilicholenga kujadili changamoto zinazohusiana na biashara ya baruti nchini.

Kikao hicho kilichofanyika leo Mei 18, 2024 katika Ofisi za Wizara jijini Dodoma, kimetumika kupokea changamoto, maoni, mapendekezo na ushauri kutoka kwa Umoja huo ambapo pia Wizara imekitumia kujibu baadhi ya hoja zilizowasilishwa huku nyingine zikipokelewa kwa ajili ya kuendelea kufanyiwa kazi.

Akizungumza katika kikao hicho, Dk Mwanga ameupongeza Umoja huo kwa kuona umuhimu wa kukutana na Wizara ili kujadili kwa pamoja masuala mbalimbali yanayohusu biashara ya baruti nchini na kueleza kuwa, vikao kama hivyo vitasaidia kujenga mahusiano mazuri ikiwemo kubaini mapungufu na changamoto katika utekelezaji wa Sheria, Kanuni na taratibu mbalimbali zinazosimamia biashara ya baruti.

" Sote tunafahamu bila biashara ya baruti hakuna uchimbaji, ninawapongeza kwa kuona umuhimu wa kukutana na sisi kujadili kwa pamoja changamoto zenu na nina amini vikao hivi vitakuwa chachu ya kufanya maboresho yanayofaa kwa Maendeleo ya Sekta hii," amesema Dkt. Mwanga.

Kwa upande wake, Katibu Mtendaji wa TEDA Mhandisi Gideon Kasege akizungumza katika kikao hicho ameipongeza Serikali kwa kuandaa Kanuni za Baruti ambazo zimeruhusu wauzaji wengi ikiwemo usafirishaji wa baruti.

Pamoja na hayo, Mhandisi Kasege ametoa angalizo kwa Serikali kuendelea na udhibiti wa biashara hiyo ambayo inaelezwa kuwa miongoni mwa bidhaa hatarishi.

Pamoja na masuala mengine yaliyowasilishwa, umoja huo umetoa ombi kwa Wizara la kuwa na mfumo wa vibali vya baruti kwa njia ya mtandao ili kuondoa changamoto za upatikanaji wake.

Wizara ya Madini imekuwa na utaratibu wa kukutana na wadau mbalimbali kwa ajili ya kujadili changamoto zinazokabili kila makundi ikiwemo wachimbaji wakubwa na wa kati, wachimbaji wadogo wa madini ya aina mbalimbali, watoa huduma migodini na wafanyabiashara wa madini kwa lengo la kujadili changamoto, kupokea maoni, ushauri na mapendekezo kwa lengo la kuendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji, shughuli za uchimbaji na biashara ya madini nchini.

Kikao hicho kimeazimia kukutana kila robo mwaka.

Jukumu la utoaji wa leseni ya biashara ya baruti ni moja ya shughuli zinazofanywa na Wizara ya Madini Makao Makuu.




NA MWANDISHI WETU, DAR

BENKI ya NMB imeingia makubaliano rasmi (MoU) na Chama cha Wanawake Wamiliki wa Shule na Vyuo Tanzania (TAWOSCO), yaliyosainiwa sambamba na uzinduzi wa ‘NMB School Proposition, lengo likiwa ni kuwawezesha kupata mikopo yenye riba nafuu kwa maendeleo ya taasisi zao.

MoU hiyo imesainiwa na Afisa Mkuu wa Fedha wa NMB, Bw. Juma Kimori na Katibu Mkuu wa TAWOSCO, Bi. Aisha Mzee, mbele ya Katibu Mkuu wa Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC), Beng'i Issa, wakishuhudiwa pia na Afisa Mkuu wa Wateja Binafsi na Biashara wa NMB, Filbert Mponzi.

Makubaliano hayo yanaleta sokoni Akaunti Maalum isiyo na Makato ya Mwezi kwa ajili ya kukusanya ada na michango mingine, Huduma ya Flex Malipo kuwezesha kukusanya malipo kupitia ‘Control Number’ na AdaBima ya kumwezesha mzazi anapopata ulemavu wa kudumu au kifo.

Akizungumza wakati wa kusaini makubaliano hayo, Bw. Kimori alisema MoU hiyo itawezesha upatikanajiwa Huduma za Wakala, Lipa Mkononi (Lipa Namba na QR), pamoja na Mashine za POS mashuleni, ambako kutakuwa na Bima za Magari, Maisha na Majengo ya Shule na mikopo mbalimbali.

Bw. Kimori alibainisha kuwa kwa kutambua kuwa Elimu Msingi Bora wa Maisha kwa Mtanzania na kwa kuthamini kazi kubwa inayofanywa na wanawake wanaomiliki shule na vyuo nchini, dhamira ya kusapoti jitihada hizo imewasukuma kusaini makubaliano hayo muhimu kwa afya ya elimu nchini.

“Mwenyekiti (wa TAWOSCO) ametuambia kaulimbiu yenu kama chama ni ‘Mwanamke Muumbaji wa Maadili,’ hili ni jambo kubwa sana, kwa sababu maadili ni jambo la lazima na tutambua kuwa shule ama chuo kikimilikwa na mwanamama, maadili mema yatakuwa kipaumbele kikuu.

“Leo hii tunasaini MoU hii tukitambua kazi kubwa iliyofanyika baina ya pande mbili hizi yaani NMB na TAWOSCO, huu mkataba unakuja na masuluhiso tele, ambayo yamejikita katika utatuzi wa changamoto na matatizo ya Sekta ya Elimu hasa shule na vyuo vya wanachama.

“Ni makubaliano yaliyobeba utatuzi wa matatizo mnayopitia wamiliki, wazazi, wanafunzi wa shule na vyo vyenu, na wadau wote, changamoto za kifedha, za mikopo, bima, ada na kadhalika, kwa hiyo mkataba huu ‘package’ iliyokamilika

“Tutatambua katika maisha, mzazi anaweza kupata ulemavu ama kifo, AdaBima iko ndani ya masuluhisho haya, lakini pia tunatambua kuwa TAWOSCO inazo taratibu za makusanyo ya michango ya wanachama, NMB imekuja na masuluhisho ya michango hiyo ya vikundi,” alibainisha Bw. Kimori.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu NEEC, Beng’i Issa ambaye alikuwa mgeni rasmi katika hafla hiyo alizipongeza NMB na TAWOSCO kwa kusaini makubaliano hayo aliyoyataja kama mkombozi wa sekta ya elimu na wamiliki wa shule na vyuo, ambao wanakabiliwa na changamoto nyingi za kifedha.

“Kuendesha taasisi za elimu kunahitaji nguvu kubwa ya kiuchumi kuweza kupata majengo, vifaa vya kuanzia biashara bila faida kwa muda mrefu, hadi kuanza kupata faida. Nawapongeza kwa sababu taasisi nyingi za kifedha zilikuwa zinakwepa kukopesha wamiliki wa shule na vyuo.

“Tatizo la fedha limekuwa kubwa sana kwenye sekta ya elimu, hasa katika shule binafsi, hawana mahali pa kupata mitaji ya kutosha kukidhi mahitaji yao, lakini naamini TAWOSCO ni taasisi nzuri kufanya nayo kazi, kwani inahusisha wanawake ambao ni kundi adilifu katika masuala ya fedha, hukopa kwa malengo na hurejesha kwa wakati.

“Leo mnaingia makubaliano na NMB, benki kwa kawaida na nadhani imeelezwa hapa kwamba watakuja kuangalia usajili wa taasisi zenu, wataangalia uzoefu wako umefanya kazi kwa miaka mingapi, wataangalia rekodi za mapato na matumizi na masuala mengine kama hayo.

“Hiyo ndio itaiwezesha benki kujua mzunguko wako wa fedha ambao ndio msingi wa ukopeshwaji, watajua uwezo wako wa kukopa na faida wanayoweza kupata kwako, kwahiyo kumbukumbu, kuweka sawa mahesabu na kukaguliwa na wakaguzi wanaotambulika ni muhimu sana,” alisisitiza Beng’i Issa.

Naye Bi. Aisha Mzee ambaye ni Katibu Mkuu wa TAWOSCO, aliishukuru NMB kwa kukubali kufanya kazi na taasisi yake, aliyosema ni moja tu kati ya taasisi nyingi ambazo NMB ingeweza kuzichagua kufanya nazo kazi, na kuwa uamuzi wa kuwachagua wao, umetuheshimisha sana.

“Kwa niaba ya wanachama wa TAWOSCO, nichukue nafasi hii kuwahakikishia NMB kwamba wanapokuwepo wanawake walio chini ya mwamvuli huu, haangushwi mtu, hapa hakitaharibika kitu.

“Tumepokea heshima zote alizotupa Afisa Mtendaji Mkuu wa NMB, uwingi wetu huu unaojumuisha wanawake kutoka mikoa mbalimbali nchini, unathibitisha namna wanavyothamini heshima waliyopewa na NMB.

“Tunawashukuru Bodi ya Wakurugenzi, Menejimenri na wafanyakazi wa NMB kwa hili, Mungu awabariki sana wote, tunaamini huko tuendako mtatupa kipaumbele wanawake ambao ndio kitovu cha maadili.

“Wito wangu kwa wanachama TAWOSCO ni kuheshimu masharti ya mikopo, raha ya mkopo ni kukopa kwa malengo na kurejesha kwa wakati. Nami nachukua dhamana kwa niaba ya wanachama hawa, nawahakikishia NMB kwamba tutasimamia uchukuaji na urejeshaji wa mikopo,” alisisitiza Bi. Aisha.







Na Janeth Raphael MichuziTv -Dodoma

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Rosemary Senyamule amesema kuwa Mkoa wa Dodoma una zaidi ya Mizinga ya nyuki 18,000 yenye uwezo wa kuzalisha zaidi ya kilo 135,000 za asali ambapo kiwango hicho bado ni kidogo ukilinganisha na fursa za ufugaji nyuki zilizopo katila mkoa huu ambapo zaidi ya hekta 1,938,193.za misitu zimehifadhiwa na zinaweza kutumika katika shughuli za ufugaji nyuki.

Senyamule ameeleza hayo mapema leo hii Jijini Dodoma katika ufunguzi wa maonesho ya siku ya nyuki Duniani ambayo kitaifa yanafanyika Jijini hapa iliyobeba kauli mbiu inayosema:NYUKI KWA AFYA NA MAENDELEO,TUWATUNZE.#APIMONDIA 2027 TANZANIA IPO TAYARI.

Na kuongeza kuwa rasilimali zilizopo katika Mkoa wa Dodoma endapo zikarumika vizuri zinaweza kuzalisha zaidi ya kilo milioni 7,000,000. za asali na kuongeza kipato cha kaya pamoja na Taifa.

"Mkoa wa Dodoma una zaidi ya mizinga 18,000 ya nyuki yenye uwezo wa kuzalisha zaidi ya kilo 135,000 za asali. Aidha, kiwango hiki bado ni kidogo ikilinganishwa na fursa za ufugaji nyuki tulizonazo kwenye mkoa wetu ambapo zaidi ya hekta milioni 1,038,193 za misitu imehifadhiwa na zinaweza kutumika kwenye shughuli za ufugaji nyuki. Pia, shughuli za ufugaji nyuki zinaweza kufanyika katika maeneo ya kilimo na kuongeza uzalishaji wa mazao ya kilimo kupitia huduma ya uchavushaji".

"Ndugu Wananchi, Rasilimali zilizopo kwenye mkoa wetu endapo zikitumika vizuri tunaweza kuzalisha zaidi ya kilo milioni 7,000,000 za asali na kuongeza kipato cha kaya pamoja na taifa".

"Hivyo, nitoe rai kwa wananchi wa mkoa wa Dodoma kuchangamkia fursa hii na kufanya shughuli za ufugaji nyuki ili kujiongezea kipato".

Aidha amesema tunapojivunia sekta hii ya nyuki katika Mkoa wa Dodoma lakini hakuna budi kutafakari uendelevu wa sekta hii kwa Mkoa na Taifa kwa ujmla ambapo zipo changamoto zinazoikabili sekta hii ikiwemo matumizi ya dawa za kuua wadudu kwenye kilimo na uchomaji moto misitu ndizo zinazotishia uendelevu wa sekta hii.

"Ndugu Wananchi;Tunapojivunia maendeleo ya sekta ya nyuki katika Mkoa wetu hatuna budi kutafakari kuhusu uendelevu wa sekta hii Mkoani hapa na Taifa kwa ujumla. Sekta ya nyuki inakabiliwa na changamoto ambazo zinatishia uendelevu wake na hivyo kuhatarisha upatikanaji wa mazao ya nyuki kwa siku zijazo. Miongoni mwa changamoto zinazotishia ukuaji wa sekta hii ni pamoja na: matumizi ya dawa za kuua wadudu kwenye kilimo, uchomaji moto misitu, kubadilisha maeneo ya ardhi ya misitu kwa matumizi mengine, kuongezeka kwa kasi ya mabadiliko ya tabia nchi ambayo yanaambatana na mabadiliko ya hewa na mazingira rafiki kwa nyuki kuzalisha mazao yao".

"Pamoja na changamoto zilizopo katika sekta ya nyuki, Mkoa wetu bado una nafasi kubwa ya kukuza na kuendeleza sekta hii. Ni wazi kuwa Mkoa wa Dodoma na Mikoa mingine bado tuna nafasi ya kuhifadhi misitu katika ardhi za Vijiji, misitu ya Halmashauri, misitu ya Serikali kuu na hifadhi za wanyamapori. Hatuna njia ya mkato ambayo itawezesha uendelevu wa mazao ya nyuki sambamba na huduma za mdudu nyuki kwenye mimea zaidi ya kumlinda na kuhifadhi mazingira yake. Niwatake wananchi wa Mkoa wa Dodoma na washiriki wa maadhimisho haya kutumia maonesho ya wadau wa sekta ya nyuki kama jukwaa muhimu la kujifunza na kukuza sekta hii kwa ajili ya kukuza uchumi wa mwananchi mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla".

Awali akitoa salamu za Wizara ya Maliasi na Utali kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara Deusdedit Boyo ambaye ni Mkurugenzi wa Idara ya Misitu na Nyuki iliyochini ya Wizara ya Maliasili na Utalii amesema kuwa Takwimu zinaonesha kuwa tuna aina mbalimbalo za nyuki zipatazo elfu 20 na pia takwimu zinaonesha kwamba karibia asilimia 90 ya mimea you duniani yenye maua inategemea nyuki.

Na kuongezea kuwa sote tu mashahidi na ni ukweli usiopingika juu ya manufaa tunayoyapata kutoka kwa nyuki iwe ni kwa kujua au kuto kujua ila tunapata manufaa ya kipekee sana.

"Takwimu zinaonesha kwamba tuna zaidi ya nyuki wapatao elfu 20 wa aina mbalimbali,pia Takwimu zinaonesha kwamba karibia asilimia 90 ya mimea yote duniani yenye maua inategemea nyuki, Takwimu zinatuonesha kwamba kadiri ya asilimia 75 ya mazao yote ya chakula yanategemea nyuki,I a maana bila nyuki tusingekuwa na mazao ya namna hii".

"Sote tu mashahidi na ni ukweli usiopingika juu ya manufaa mengi tunayoyapata kutoka kwa mdudu nyuki iwe kwa kujua ama kwa kutokujua tumenufaika kwa namna ya kipekee na mazao yao mbalimbali yanayozalishwa na nyuki".

Kilele cha maonesho haya ya siku ya Nyuki Duniani itakuwa ni May 20,2024, ambapo inafanyika Dodoma na Mgeni Rasmi anatarajiwa kuwa Makamu wa Raisi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania p Dkt Philip Mpango.






NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM

Jumuiya ya Mitandao ya Kijamii Tanzania (JUMIKITA) kwa kushirikiana na Shirikisho la Serikali za Wanafunzi wa Vyuo Vikuu Tanzania (TAHLISO) wameandaa kongamano la waandishi wa habari wa vyombo vya mitandao ya kijamii nchini kwa lengo la kuimarisha wigo wa utoaji wa habari kupitia mitandao ya kijamii na mipango mbalimbali ya maendeleo.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika kongamano hilo linalotarajiwa kufanyika Jumatatu Mei 20, 2024 katika ukumbi wa maktaba katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).

Akizungumza na waandishi wa habari leo Mei 18, 2024 Jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa JUMIKITA Shaaban Matwebe amesema Kongamano hilo linatarajiwa kuwa na washiriki zaidi ya 500, ambapo mada mbalimbali zitajadiliwa ikiwa ni pamoja na mitandao ya kijamii na uzalendo, fursa zilizopo kwenye tasnia hiyo, mafanikio na changamoto ili kutoa mchango wa kiundeshaji kwa wadau kupitia JUMIKITA.

"Tutatoa pia mapendekezo yatakayosaidia serikali kwenye uratibu wa sera za jinsi ya kuunganisha sayansi ya uchumi wa taarifa (information economics) na uchumi wa taarifa (information economy)". Amesema

Aidha amesema kuwa Kongamano hilo litajadili mafanikio ya miaka mitatu ya serikali ya Dkt. Samia Suluhu Hassan ikiwa ni pamoja na maadhimisho ya siku ya uhuru wa habari duniani.
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Mitandao ya Kijamii Tanzania (JUMIKITA), Shaaban Matwebe akizungumza na waandishi wa habari wakati akitoa taarifa ya ujio wa Kongamano la Waandishi wa Habari wa mitandao ya Kijamii litakalofanyika Mei 20,2024 katika ukumbi wa Maktaba Mpya Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam ambapo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa  Kassim Majaliwa.
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Mitandao ya Kijamii Tanzania (JUMIKITA), Shaaban Matwebe akizungumza na waandishi wa habari wakati akitoa taarifa ya ujio wa Kongamano la Waandishi wa Habari wa mitandao ya Kijamii litakalofanyika Mei 20,2024 katika ukumbi wa Maktaba Mpya Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam ambapo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa  Kassim Majaliwa.

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Mitandao ya Kijamii Tanzania (JUMIKITA), Shaaban Matwebe akizungumza na waandishi wa habari wakati akitoa taarifa ya ujio wa Kongamano la Waandishi wa Habari wa mitandao ya Kijamii litakalofanyika Mei 20,2024 katika ukumbi wa Maktaba Mpya Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam ambapo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa  Kassim Majaliwa.

(PICHA ZOTE NA EMMANUEL MBATILO)

Arusha 18 Mei 2024 - Wanahisa wa Benki ya CRDB wameidhinisha kwa kauli moja mapendekezo ya Bodi ya Wakurugenzi kuhusu malipo ya gawio la Shilingi 50 kwa kila hisa jambo linalofanya jumla ya thamani ya gawio la mwaka wa fedha 2023 kufikia Shilingi bilioni 130.6, sawa na 30.9% ya faida halisi.

Katika taarifa yake wakati wa Mkutano Mkuu wa 29 wa Benki hiyo uliofanyika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Arusha (AICC), Mwenyekiti wa Bodi ya Benki hiyo Dkt. Ally Laay alisema gawio lililoidhinishwa kwa kila hisa ni ongezeko la asilimia 11 ikilinganishwa na Shilingi 45 kwa kila hisa iliyotolewa jana, ikiashiria ukuaji mkubwa wa mapato kwa kila hisa kufikia Shilingi 161.9 ikilinganishwa na Shilingi 134.1 mwaka 2022.
"Kwa mara nyingine tena, tunafuraha kuwatoa thamani endelevu kwa wanahisa wetu. Utendaji wa Benki mwaka 2023 ulikuwa mzuri, ikiwa ni uthibitisho wa mafanikio ya mkakati wetu mpya wa miaka mitano wa muda wa kati wa 2023 - 2027. Benki yetu na kampuni zake tanzu ilipata faida halisi ya Shilingi 422.8 bilioni, ongezeko la 20.3%," alisema Dkt. Laay.

Alibainisha zaidi kuwa kampuni tanzu za Benki ya CRDB zilitoa mchango chanya kwa mwaka uliopita. CRDB Bank Burundi ilipata ukuaji mzuri wa 30.7% katika Faida Baada ya Kodi, na kufikia Shilingi 30.2 bilioni. Amesema pamoja na kampuni za CRDB Bank Congo na CRDB Insurance Company Ltd kutotengeneza faida, kampuni hizo zimeonyesha mwanzo mzuri unaoashiria kuwa na mchango mkubwa katika siku za usoni. Jumla ya mchango wa kampuni tanzu kwenye Faida Baada ya Kodi ulikuwa 6%.
"Ninafurahia kuona juhudi zetu za upanuzi za kikanda zinaleta matokeo chanya. CRDB Bank Burundi imefanikiwa kuongoza kwa faida katika soko la nchi hiyo katika kipindi cha robo ya kwanza ya 2024. Zaidi ya hayo, kampuni yetu ya nchini DRC imepokelewa vizuri nchini humo tangu kuanzishwa kwake mwezi Julai 2023, na kuvutia wateja na biashara nyingi nchini humo,” aliongeza.
Afisa Mkuu wa Fedha, Fredrick Nshekanabo, aliripoti kuwa Mizania ya Benki ya CRDB na kampuni zake tanzu imeendelea kuimarika ikishuhudia ukuaji wa mwaka wa 14.5% kutoka shilingi trilioni 11.6 mwaka 2022 mpaka shilingi trilioni 13.3 mwaka 2023. Ukuaji huo ulichangiwa zaidi na ongezeko la 22.8% la mikopo kufika shilingi trilioni 8.4 ikichangiwa na ongezeko la amana za wateja zilizopanda kwa 8.0%, mikopo kwa 73.9%, na kukua kwa mtaji wa wanahisa kwa 20.4%. 
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela amesisitiza kuwa mkakati mpya wa biashara umekuwa muhimu kwa mafanikio ya benki, ukifanya kazi kama ramani ya kuboresha utendaji kazi. Amesema kwa sehemu kubwa Benki ya CRDB ilijikita katika uwekezaji kwenye mifumo ya kidijitali, huku akieleza kuwa benki imepiga hatua kubwa katika utekelezaji wa mradi wa mfumo mkuu mpya wa uendeshaji wa benki (CBS).

Nsekela pia alisema kuwa Benki ya CRDB imewekeza kwa kiasi kikubwa katika kukuza ujumuishi wa kifedha, kwa wajasiriamali na wafanyabiashara. Kupitia mpango wa IMBEJU taasisi ya CRDB Bank Foundation imeboresha uwezeshaji kwa vijana na wanawake. Zaidi ya hayo, Benki imeunda ushirikiano wa kimkakati ili kufadhili vyema miradi ya maendeleo nchini.
Nsekela alielezea mipango ya siku za usoni ya Benki ya CRDB na kampuni zake, akisisitiza kuongeza kwa mchango wa kampuni tanzu zilizoanzishwa, kuboresha huduma kwa wateja na kuwekeza zaidi katika ubunifu wa kidijitali. Kadhalika, amesema Benki hiyo itaendelea kuongeza usimamizi mkubwa katika vihatarishi, na kuhakikisha inaendana na mabadiliko ya usimamizi, na kuhakikisha utawala bora.

Kwa upande mwingine, Wanahisa wa Benki ya CRDB waliidhinisha kampuni ya Price Water Coopers (PWC) kama Wakaguzi wa Nje wa Benki kwa mwaka wa fedha wa 2024. Wanahisa wa Benki pia walichagua tena Wajumbe wawili wa Bodi, Prof. Faustine Bee kuwakilisha wanahisa wenye umiliki chini ya 1%, na Gerald Kassato kuwakilisha wanahisa wenye hisa kati ya 1% na 10%.
Akizungumzia malipo ya gawio hilo, aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Benki hiyo na Mbunge wa Vunjo, Dkt. Charles Kimei, alieleza kufurahishwa kwa wanahisa kwa kuendelea kupata ongezeko la gawio, akibainisha kuwa hisa za benki hiyo zimebakia kuwa chachu ya wawekezaji kwasababu benki haijawahi kushindwa kulipa gawio kwa wanahisa wake.










Top News