Na. Dennis Gondwe, KIWANJA CHA NDEGE

WANANCHI wa Mtaa wa Osterbay, Kata ya Kiwanja cha Ndege Halmashauri ya Jiji la Dodoma wamejitokeza kufanya usafi wa mazingira katika eneo la Shule ya Msingi Mlimwa B kwa lengo la kuweka mazingira safi na kuepuka na magonjwa ya mlipuko kwa wanafunzi na jamii kwa ujumla.

Kauli hiyo ilitolewa na Afisa Mtendaji Mtaa wa Osterbay, Ashura Iberia alipokuwa akiongea na wananchi wa Mtaa wa Osterbay waliojitokeza kwa wingi kufanya usafi wa mazingira katika Shule ya Msingi Mlimwa B.

Iberia alisema “leo tumefanya usafi wa mazingira kuzunguka Shule ya Msingi Mlimwa B, wananchi wa Mtaa wa Osterbay wamejitokeza kwa wingi kufanya usafi wa mazingira. 

Lengo la kufanya usafi huo ni kuweka mazingira ya shule safi ili wanafunzi ambao ni watoto wetu wasome katika mazingira safi na salama. Lakini pia kuwaepusha wanafunzi na jamii inayozunguka shule hii na magonjwa ya mlipuko. Zoezi hili nimelisimamia mimi mwenyewe Afisa Mtendaji Mtaa wa Osterbay ili kutoa chachu na hamasa kwa usafi wa mazingira kwa kila mwananchi”.

Kwa upande wake, Kaimu Mwenyekiti wa Mtaa wa Osterbay, Hussein Ngura alisema kuwa kuanzia siku hiyo usafi ni agenda ya mtaa. “Kuanzia leo agenda yetu kuu ya Mtaa wa Ostebay ni usafi wa mazingira kama alivyosema Afisa Mtendaji wa Mtaa. Kama tutakumbuka aliwahi kufika hapa Mkuu wa Wilaya ya Dodoma na kukagua usafi kwa kustukiza. 

Sasa hatujui ni kiongozi gani atafuata kuja kukagua, hivyo lazima tujipange kwa kuweka mazingira yetu safi. Wananchi wa Mtaa wa Osterbay mmenitendea imani kuwa nina watu kwa jinsi mlivyojitokeza kwa wingi kushiriki zoezi hili la usafi wa mazingira. Pia, mimi namsifu sana Afisa Mtendaji wa Mtaa wetu kwa kazi nzuri anayofanya, hakika ni mchapa kazi hodari na anatuongoza vizuri” alisema Ngura.

Zoezi la usafi wa mazingira katika Mtaa wa Osterbay, Kata ya Kiwanja cha Ndege liliongozwa na Afisa Mtendaji wa Mtaa, na kuhudhuriwa na wenyeviti, mabalozi na mamia ya wananchi.




Halmashauri ya mji wa Njombe mefanikiwa kutoa chanjo ya Saratani ya mlango wa kizazi kwa wasichana wenye umri kati ya 9 - 14 kwa 91% na kuvuka lengo la angalau 80% kitaifa huku wakitarajia kufikia 100% ifikapo Mwezi Disember 2024 mwaka huu ili kujikinga na maambukizi ya ugonjwa huo.

Simon Ngassa ni mtaalamu wa afya ambaye ni mratibu wa chanjo wa halmashauri hiyo akizungumza na vyombo vya habari amesema licha ya changamoto kadhaa walizopitia katika zoezi hilo lakini wamefanikiwa kwa kiasi kikubwa kutoa chanjo kwa mabinti wengi kupitia shuleni na mikutano ya hadhara baada ya elimu kutolewa.

"Halmashauri ya mji Njombe tumefanikiwa kufikia 91% na kuvuka lengo lile ambalo tulikuwa tumepewa angalau 80% kitaifa hivyo tunaendelea kutoa huduma,na hawa ambao wataendelea kupata kwenye utaratibu wa kawaida ni matarajio yetu inapofika mwezi Desember mwaka huu nao wataingia kukamilisha asilimia hizi ambazo zimebaki"amesema Ngassa

Aidha Ngassa amesema halmashauri bado ina chanjo za kutosha ambapo ametoa wito kwa walengwa kuendelea kufika kwenye vituo vya afya kwa ajili ya chanjo hiyo.

"Tunatoa wito kwa wazazi kwamba huduma hii ya kutoa chanjo inaendelea kwenye vituo vyetu kwa wasichana wale ambao hawakuweza kupata chanjo ili inapofika mwezi Disember wasichana wote wawe wamekingwa dhidi ya saratani ya mlano wa kizazi kwa hiyo chanjo zipo kwenye vituo vyote vya kutoa huduma za afya"aliongeza Ngassa




Na Fauzia Mussa Maelezo.05.05.2024.

Mkuu wa Oganaizesheni Afisi Kuu ya chama cha mapinduzi Zanzibar Omar Ibrahim Kilupi amezitaka jumuiya za chama cha Mapinduzi kuweka mikakati ya kuwatambua vijana ambao hawajasaliliwa katika datfari la wapiga kura ili waweze kusajiliwa.

Akifungua kongamano la jumuiya ya wazazi wa Mkoa wa Magharibi Kichama huko Skuli ya Ali Hassan Mwinyi Bububu amesema kuna baadhi ya vijana hawakujiandikisha katika awamu iliopita hivyo ni vyema kuwatambua na kuwahamasisha kujiandikisha katika awamu ijayo.

Amezitaja baadhi ya sababu zilizopelekea vijana hao kutojisajili kuwa ni pamoja na kutotimiza umri wa miaka 18 pamoja na kuwa mbali na vituo vya kujiandisha kwa kipindi hicho.

Aidha amezitaka jumuiya hizo, kuhakikisha vijana wote waliotimiza vigenzo wanajisajili ili kuweza kupata vijana wengi watakaoendelea kukiweka madarakani chama cha Mapinduzi ifikapo 2025.

“Kuna kundi la wananchi ambao wana sifa za kujisajili lakini hawajaenda kujisajili na kama tunavyojuwa kama hukujisajili katika daftari la kudumu la wapiga kura hutoweza kupiga kura, tuendeni tukahamasishe ili tusije kumuacha mtu nyuma.” alisema Kilupi.

Aidha amesema lengo la mafunzo hayo ni kutoa elimu ya uchaguzi na mmongonyoko wa maadili na kuwataka kuyafanyia kazi mafunzo walipopewa sambamba na kuwa mabalozi wazuri kwa wenzao.

Kwa upande wake Mlezi wa Mkoa wa magharibi kichama ambae pia Mwakilishi wa viti maalum kupitia jumuiya ya wazazi mkoa wa kusini Unguja Mhe. Sabiha Filfil Thani amesema kuna kila sababu ya Dkt. Hussein Ali Mwinyi kuendelea kubaki madarakani katika Uchaguzi unaotarajiwa kufanyika hapo mwakani kutokana na kutekeleza kwa vitendo ilani ya chama hicho.

“Ilani ya CCM ilimtaka rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kujenga madarasa 1,500 kwa Skuli za Unguja na Pemba ambapo amevunja rikodi kwa kujenga madarasa 2273 sawa na silimia 150 ya malengo ya ilani ya chama cha Mapinduzi.” amefahamisha Mlezi huyo.

Katika kongamano hilo mada mbili ziliwasilishwa na kujadiliwa ikiwemo mmongonyoko wa maadili na uchaguzi Mkuu ambapo Kauli mbiu ni ”USHINDI WA CCM 2024-2025 JUMUIYA YA WAZAZI TUPO MSTARI WA MBELE”







Na; Mwandishi Wetu – Songea

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya (Sera, Bunge na Uratibu), Mhe Jenista Mhagama amezindua Mradi wa kuendeleza lishe na ufugaji endelevu wa viumbe maji kwa wakulima wadogo (ARNSA) katika kijiji cha Mpitimbi kilichopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Songea Vijijini Mkoani Ruvuma Tarehe 4 Mei 2024.

Mradi huo wa kuendeleza lishe na ufugaji endelevu wa viumbe maji kwa wakulima wadogo (ARNSA) unaoenda kutekelezwa katika Wilaya nne za Mikoa ya Ruvuma na Lindi, na kulenga katika kunufaisha kaya elfu Moja (1000) katika Wilaya za Songea vijijini, Mbinga Mkoani Ruvuma, Ruhangwa na Mtama Mkoani Lindi, ambapo pamoja na mambo mengine Familia na jamii hizo zinaenda kuinua hali ya maisha kwa kuongeza kipato na kuimalisha Lishe.

Akiongea katika uzinduzi wa mradi huo,Waziri Mhagama alisema Mpitimbi imebahatika kuanza na mradi huu, na kwakuwa Mkoa wa Ruvuma unaongoza kwa uzalishaji wa mazao ya chakula lakini, una changamoto ya udumavu,”Na ndiyo maana Serikali imeleta mradi huu ambao utatumia takribani zaidi ya shilingi Bilioni tatu nukta moja, katika maeneo tuliyojipangia, ambao ni sehemu ndogo tuu ya Programu kubwa ya kuendeleza sekta ya Kilimo na Uvuvi, Tumebahatika kuanza na mradi huu unaofadhiliwa na ubalozi wa Norway Nchini hivyo ni wakati mzuri wa Wilaya zitakazonufaika kuweza kujikimu kimapato na kiafya.” Alisema.

Aliendelea kusema kuwa, kwa kuwa hali ya udumavu inaleta changamoto ya afya ya akili ni fursa sasa kwa wananchi wa mkoa wa Ruvuma kuendelea kuboresha afya, kupitia lishe ya viumbe maji na hasa Samaki.

Waziri Mhagama aliushukuru ubalozi wa Norway kupitia shirika lake la NORAD kuleta mradi huo mkoani Ruvuma, “Leo Tunazindua Shamba Darasa Ambalo linaenda kuchagiza maendeleo ya tabianzuri ya biashara na matumizi ya lishebora kupitia samaki wanaofugwa kwenye mabwawa, na miradi itakayofanywa kwenye baadhi ya halmashauri za Mkoa wa Ruvuma.” Alisisitiza.

Alibainisha kuwa, Kupitia bwawa kubwa la Asili lililopo Mpitimbi ni wakati sahihi sasa wa kuimarishwa kwa bwawa hilo na kuanza kwa ufugaji mkubwa wa Samaki “Tunatamani kuona kuwa Bwawa hilo lenye ukubwa wa hekari 17.4 linaendelezwa na kuwa shamba Darasa.” Alisema

Awali, Waziri Mhagama Alimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa, kupeleka Miradi mingi ya Maendeleo katika Mkoa wa Ruvuma.

Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu wa Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Bw. Anderson Mutatembwa alisema, kupitia mradi huo unaoenda kutekelezwa kwa miaka miwili,Tanzania imekuwa Miongoni mwa nchi tatu za Afrika kupata bahati ya kunufaika na Mradi huo, zikiwemo nchi za Kenya na Msumbiji.

Aliendelea kusema kuwa, mradi huo wa kuendeleza Lishe na ufugaji endelevu wa viumbemaji na ukulima wa mwani kwa wakulima wadogo unatekelezwa katika mikoa kumi na moja ya Tanzani Bara pamoja visiwa vya unguja na Pemba.

Akiongea katika ghafla hiyo muwakilishi kutoka Mfuko wa Kimataifa wa maendeleo ya Kilimo nchini (IFAD) Bi. JacquiIine Machangu Motcho aamesema, IFAD imekuwa ikifanya kazi kwa ushirikiano mkubwa na Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania katika nyanja na sekta zinazolenga, kutatua changamoto mbalimbali zinazoikumba sekta ya kilimo hususani Wakulima wadogo wadogo hasa wale walio vijijini.

Na aliendelea kusema kuwa, Shirika hilo limeendelea pia kuyapa kipaumbele maeneo hayo ikiwa na dhamira ya kuinua na kuboresha sekta ya Kilimo, Mazao, Mifugo na Uvuvi ili kufikia uzalishaji wa juu ulio endelevu na wenye faida kibishara, unaoleta ukuaji wa pamoja kiuchumi na Taifa zima kwa ujumla.

Akizungumza kuhusu mradi huo, Bi JacquiIine alisema Kupitia Programu ya kuendeleza Kilimo na Uvuvi, IFAD imepokea ufadhili-ruzuku(grant) kwa mradi wa ARNSA kutoka Ubalozi wa Norway, unaolenga kupunguza umaskini na kuboresha lishe kupitia shughuli za Ufugaji wa Samaki wenye tija na ustahimilivu kutoka kwa wazalishaji/wafugaji wadogo. Dhamira yake ya kimaendeleo inalenga kuongeza mapato, kujenga ustahimilivu na kuwajengea uwezo kimaisha wafugaji wadogo wa samaki walio vijijini.


Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Mhe. Jenista Mhagama akizungumza katika Uzinduzi wa mradi wa kuendeleza lishe na ufugaji endelevu wa viumbe maji kwa wakulima wadogo (ARNSA), uliyopo chini ya Progamua ya Kuendeleza Kilimo na Uvuvi (AFDP), katika kijiji cha Mpitimbi Wilayani Songea Vijijini Tarehe 4 Mei, 2024
Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Bw. Anderson Mutatembwa, akitoa Neno la Utangulizi wakati wa Uzinduzi wa mradi wa kuendeleza lishe na ufugaji endelevu wa viumbe maji kwa wakulima wadogo (ARNSA), uliyopo chini ya Progamua ya Kuendeleza Kilimo na Uvuvi (AFDP), katika kijiji cha Mpitimbi Wilayani Songea Vijijini Tarehe 4 Mei, 2024

Picha ikionesha Baadhi ya washiriki wakati wa Uzinduzi wa mradi wa kuendeleza lishe na ufugaji endelevu wa viumbe maji kwa wakulima wadogo (ARNSA), uliyopo chini ya Progamua ya Kuendeleza Kilimo na Uvuvi (AFDP), katika kijiji cha Mpitimbi Wilayani Songea Vijijini Tarehe 4 Mei, 2024
Muwakilishi kutoka Mfuko wa Kimataifa wa Maendeleo ya Kilimo nchini (IFAD) Bi. JacquiIine Machangu Motcho, akizungumza wakati wa Uzinduzi wa mradi wa kuendeleza lishe na ufugaji endelevu wa viumbe maji kwa wakulima wadogo (ARNSA), uliyopo chini ya Progamua ya Kuendeleza Kilimo na Uvuvi (AFDP), katika kijiji cha Mpitimbi Wilayani Songea Vijijini Tarehe 4 Mei, 2024
Aliyeinama, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Mhe. Jenista Mhagama, akiweka mbegu ya Samaki katika moja ya Bwawa, wakati wa Uzinduzi wa mradi wa kuendeleza lishe na ufugaji endelevu wa viumbe maji kwa wakulima wadogo (ARNSA), uliyopo chini ya Progamua ya Kuendeleza Kilimo na Uvuvi (AFDP), katika kijiji cha Mpitimbi Wilayani Songea Vijijini Tarehe 4 Mei, 2024


Picha ya pamoja Baadhi ya washiriki, baada ya Uzinduzi wa mradi wa kuendeleza lishe na ufugaji endelevu wa viumbe maji kwa wakulima wadogo (ARNSA), uliyopo chini ya Progamua ya Kuendeleza Kilimo na Uvuvi (AFDP), katika kijiji cha Mpitimbi Wilayani Songea Vijijini Tarehe 4 Mei, 2024

Na Munir Shemweta, MLELE

Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi na Mbunge wa jimbo la Kavuu katika halmashauri ya Mpimbwe wilaya ya Mlele mkoa wa Katavi Mhe, Geophrey Pinda amekabidhi gari la wagonjwa kwa ajili ya Kituo cha Afya Kibaoni.

Mhe, Pinda amekabidhi gari hiyo tarehe 4 Mei 2024 katika hafla maalum iliyofanyika eneo la Kibaoni na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa wilaya ya Mlele akiwemo Mkuu wa wilaya hiyo Alhaji Majid Mwanga na Mkurugenzi wa halmashauri ya Mpimbwe Bi. Shamim Daud.

Kukabidhiwa kwa gari hilo kunaifanya halmashauri ya Mpimbwe kuwa na jumla ya magari matatu ya kubebea wagonjwa yanayohudumia vituo vya afya vya Kibaoni na Usevya huku gari moja ikihudumia hospitali ya wilaya ya Tupindo.

Akizungumza wakati wa kukabidhi gari hilo, Mbunge wa Jimbo la Kavuu na Naibu Waziri wa Ardhi Mhe, Pinda amewaomba wananchi wa kibaoni kuitumia gari hiyo kwa manufaa yao huku akimtaka mkurugenzi wa halmashauri ya Mpimbwe kuhakikisha gari waliyokabidhiwa inabakia kwa matumizi ya kituo hicho cha afya cha Kibaoni.

‘’Gari ya Kibaoni ikae kibaoni na kule Mamba nikuombe vile vile apatikani dereva haraka na akae pale gari inapolala kwa sababu magari haya siyo mapambo na ni huduma muhimu kwa wananchi’’ alisema Mhe, Pinda

Ameweka wazi kuwa, gari hilo linaenda kuongeza uwezo kwa kituo hicho cha afya kwa kuwa mtu akipata rufaa kutoka Kibaoni kwenda Hospitali ya wilaya mafuta hayatatumika sana tofauti na hapo awali ambapo ililazimika mgonjwa kupelekwa sumbawanga.

Upatikanaji gari la wagonjwa kwenye Kituo cha Afya Kibaoni kutasaidia kutatua changamoto za usafiri sambamba na kurahisisha huduma za dharura kwa maeneo jirani na hiyo inatokana na kuongezeka kwa mahitaji katika eneo la Kibaoni kama vile uwepo wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) Kampasi ya Mizengo Pinda.

Mhe, Pinda amewaeleza wananchi wa Kibaoni kuwa, gari iliyokabidhiwa ni mali yao na itatumika kwa kazi za dharura hasa wagonjwa na sasa hakutakuwa tena na ulazima wa kukodi bajaji kwa ajili ya kusafirisha wagonjwa walio katika hali hatarishi na atabebwa na gari hiyo ku[elekwa mahali ambapo madaktari wamependekeza kupelekwa.

Wananchi wa Kibaoni wamemshukuru Mbunge wa jimbo la Kavuu Mhe, Geophrey Pinda kwa kusaidia upatikanaji wa gari hilo la wagonjwa pamoja na fedha za ujenzi wa kituo cha afya cha Kibaoni.

Kwa mujibu wa taarifa ya halmashauri ya Mpimbwe, mwezi Januari 2024 kituo hicho kilipokea shilingi milioni 175 kutoka serikali kuu kwa ajili ya ununuzi wa vifaa tiba pamoja na umaliziaji majengo ya Maabara, Jengo la Mama na Mtoto, Upasuaji na Kichomea Taka.

Ukamilishaji wa kituo cha Afya Kibaoni utatoa huduma kwa wananchi takriban 28,817 wa kata ya kibaoni na viunga vyake.
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi na Mbunge wa jimbo la Kavuu katika halmashauri ya Mpimbwe Mhe, Geophrey Pinda akikata utepe kuzindua gari la kubebea wagonjwa la Kituo cha afya cha Afya Kibaoni tarehe 4 Mei 2024.
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi na Mbunge wa jimbo la Kavuu katika halmashauri ya Mpimbwe Mhe, Geophrey Pinda akimkabidhi fungua ya gari la wagonjwa Mkurugenzi wa halmashauri ya Mpimbwe Bi Shamim Daudi tarehe 4 Mei 2024.
Mbunge wa jimbo la Kavuu na Naibu Waziri wa Ardhi Myumba na Maendeleo Mhe Geophrey Pinda (katikati), Mkuu wa wilaya ya Mlele Alhaji Majid Mwanga (aliyevaa tai), Mkurugenzi wa halmashauri ya Mpimbwe Bi. Shamim Daud (aliyenyoosha funguo) na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mpimbwe Silas Ilumba (kushoto) wakifurahia mara baada ya makabidhiano ya  gari la wagonjwa kwa ajili ya kituo cha Afya Kibaoni tarehe 4 Mei 2024.
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi na Mbunge wa jimbo la Kavuu katika halmashauri ya Mpimbwe Mhe, Geophrey Pinda akizungumza na wananchi wa Kibaoni mara baada ya kukabidhi gari la wagonjwa kwa kituo cha afya kibaoni tarehe 4 Mei 2024.
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi na Mbunge wa jimbo la Kavuu katika halmashauri ya Mpimbwe Mhe, Geophrey Pinda akiwaongoza viongozi wengine kwenda kukabidhi gari la wagonjwa kwa kituo cha Afya Kibaoni tarehe 4 Mei 2024.

Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa, ameeleza kuwa timu ya watalaamu wa Wakala ya Barabara (TANROADS) na Makandarasi itatumia saa 72 (siku 3) kukamilisha zoezi la kurejesha miundombinu ya barabara ya Lindi – Dar es Salaam, ambayo imeharibiwa na mvua kubwa zinazoendelea kunyesha zilizombatana na kimbunga Hidaya.

Amesema hayo Mkoani Lindi Mei 05, 2024, mara baada ya kuwasili na kukagua uharibifu wa miundombinu ya barabara ya Lindi - Dar es Salaam na kuzungumza na wananchi na wasafiri wa Mikoa ya Mtwara, Lindi, Ruvuma, na Dar es Salaam wanaotumia barabara hiyo na kutoa pole na kuwataka kuwa wavumilivu wakati Serikali ikiendelea na jitihada za kujereshwa miundombinu.

“Mitambo ipo inaletwa hapa, kazi ya kurudisha mawasiliano ya barabara hii itaanza wakati wowote kuanzia sasa, ni lazima tuanze na kipande kimoja ili tuweze kufika katika maeneo mengine yaliyoathiriwa. Namna miundombinu imeharibika na tathmini iliyofanyika tunahitaji masaa yasiyopungua 72 ili kuweza kurudisha mawasiliano,” amefafanua Bashungwa.

Bashungwa ameeleza kuwa mawasiliano ya barabara hiyo yamekatika katika maeneo matano ambayo ni pamoja na eneo la barabara ya Somanga – Mtama, eneo la Mikereng’ende kutokea Somanga na eneo la Lingaula kutokea Lindi.

Aidha, Bashungwa amewahakikishia wananchi kuwa Serikali itafanya kila jitihada ili ifikapo Jumatano jioni mawasiliano ya barabara hiyo yarejee katika hali yake.

Naye, Mkuu wa Wilaya ya Kilwa, Mohamed Nyundo ameeleza kuwa maji yaliyokuwa yakipita juu ya barabara yalizidi kiwango na kusababisha madaraja kushindwa kuhimili wingi na kasi ya maji na hivyo kusababisha uharibifu mkubwa katika maeneo matano ikiwemo Somanga, Mikereng’ende, na Lingaula.

Nyundo amemueleza Waziri Bashungwa kuwa kazi ya awali iliyofanyika ni kuwasiliana na taasisi zinazohusika kwa Mkoa wa Ruvuma, Mtwara na Lindi ili kutoa taarifa kwa wasafirishaji na watumiaji wa barabara hiyo kusimamia safari zao mpaka pale miundombinu itakaporejeshwa katika hali yake.








*Awashangaa kumchonganisha Rais Samia kwasababu tu ni Mzanzibar

*Apangua hoja Kuhusu madai Katiba mpya,Sheria mpya ya uchaguzi


Na Said Mwishehe, Dodoma


MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Abdulrahman Kinana ameshauri wananchi kutokubali hoja za kejeli, chuki na kugombanisha watu zinazotolewa na CHADEMA.

Pia Kinana amesema viongozi wa CHADEMA kwa katika mikutano yao ya hadhara wamekuwa wakieneza chuki na kumchanganisha Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa hoja dhaifu kwamba anatoka Zanzibar na amekuwa anaihujumu Bara.

Akizungumza leo Mei 5,2024 Wana CCM pamoja na wananchi alipokuwa katika mkutano maalumu wa CCM Mkoa wa Dodoma, Kinana amesema CHADEMA katika mizunguko yao wameituhumu CCM, Serikali na Rais kwa hoja za uongo.

"Hatukatai kukoselewa, hatukatai kusahihishwa, lakini hatukubali kuzuliwa au kushutumiwa kwa mambo ambayo hayapo. Kubwa ambalo wamefanya ni kujenga chuki miongoni mwa Watanzania, kujenga mifarafakano.

"Wakaenda mbali zadi wakaanza kuzusha jambo ambalo wanataka kuifanya ajenda, wanasema nchi ina Rais ambaye ni Mzanzibari na anaihujumu Bara, lakini ajenda hiyo imeshindwa."

Ameongeza CHADEMA wanazungumza kuhusu Rais Samia ni Mzanzibar, hana huruma na Bara, hana jema analofanya kwa Bara, hana msaada.

“Wanataka kumtenganisha Rais na Watanzania, nani amekataa kwamba Rais Samia sio Mzanzibari. Ni Mzanzibari na ametokana na Katiba ambayo inaeleza mgombea urais akitoka Zanzibar basi mgombea mwenza anatoka upande wa pili…

“Ndivyo tulivyokubaliana na huyu ni mgombea mwenza ana nafasi sawa na mgombea urais. Ikitokea mgombea mwenza hayuko uchaguzi unaahirishwa. Mwaka 2005 uchaguzi uliahirishwa kwa sababu mgombea mwenza wa CHADEMA alifariki dunia.

“Halafu leo wanakejeli kiongozi kutoka Zanzibar, wametafuta namna ya kushughulika na Rais (Dk. Samia) lakini wakiangalia barabara zinajengwa, bwawa la mwalimu Nyerere limefika pazuri, ujenzi wa mji wa Dodoma unaendelea kwa kasi.

“Reli ya mwendo kasi sasa imefika Dodoma na ujenzi unaendelea sasa wanakosa hoja wanakuja na maneno ya kuzusha kwamba Rais hafai kwa sababu anatoka Zanzibar. Rais Samia ni Rais wa katiba amechukua uongozi baada ya Rais Dk. John Magufuli kufariki dunia,” alisema.

Ameongeza kwamba “Rais Samia alikuwa Mgombea Mwenza akawa Makamu wa Rais, na awamu ya pili Magufuli akamteua tena lakini oooh… huyo Mzanzibar ili watu baadae polepole waanze kusema tunatawaliwa na Mzanzibari.”

Amewaomba Watanzania kupuuza uzushi huo na kushauri wasimame na Rais Samia kwani anafanya kazi nzuri.

"Tangu awamu mbalimbali zilizopita kuna sera iliyoanza baada ya Mzee Mwinyi kuchukua nchi kwa kuanzisha sera ya sekta binafsi kushiriki kukuza uchumi.

“CHADEMA wanasema Rais Samia anauza kila kitu, kauza nini?. Awamu ya Tatu Rais mstaafu Benjamin Mkapa alibinafsisha mashirika zaidi ya 200 kwani alikuwa Mzanzibar?

“Wakati TICS wanapewa bandari ya Dar es Salaam nchi haikuuzwa, lakini baada ya kupewa DP World nchi inauzwa. Hivi mnaamini kweli Rais anaweza kukaa na kufanya jambo ambalo halina nia njema na nchi yetu.

“Rais haamui peke yake kuna vyombo ambavyo vinakaa na kuangalia mambo na kisha vinamshauri Rais. Kataeni juhudi zinazofanyika za kujenga chuki dhidi ya Rais. Kuna wakati Shirika la Reli Tanzania (TRC) lilikabidhiwa kwa RITES (kampuni) kutoka India? Alikabidhi Rais Samia?”

Kinana amesema hayo mambo yanafanyika kwa malengo na hasa kuleta tija na ufanisi, hivyo Watanzania wasikubali kusikiliza hoja rejareja, hoja za msimu.

Pia amesema Rais Samia ambaye wanamsema ndiye ameleta uhuru wa kusema, kushutumu, kuandamana. Mikutano ya hadhara wanaweza kusema iko katika Katiba lakini huko nyuma wakati wananyimwa kwani haikuwepo kwenye Katiba?.

“Katiba ilikuwepo, uhuru ulikuwepo lakini walikatazwa kwenda barabarani. Amekuja Rais muungwana ameondoa kifungo. Akisema kuanzia leo hakuna maandamano, watafanya? Wanamkejeli na kumtuhumu Rais amekaa kimya.

“Waamuzi ni wao. Wana CCM dawa yao kwenye sanduku la kura, wenzetu wanatafuta nguvu katika sanduku la kura. Watanzania hawapendi kejeli. Nina uhakika adhabu watakayopata watajutia.

Kuhusu hoja ya Katiba, sheria mpya ya uchaguzi na muungano Kinana amesema kwamba ukisikiliza kwa makini utabaini wanataka kuleta mfarakano kati ya bara na Zanzibar.

“Wamekuwa wakizunguka na ajenda ya kuligawa taifa katika majimbo, hii ni sera ambayo wamekuwa nayo kwa muda. Msimamo wa CCM Watanzania tusikubali kugawanywa kwa namna yoyote,” amesema Kinana.

Akizungumzia Katiba mpya ,Kinana amesema kulifanyika mazungumzo kwa mwaka mzima baina ya CHADEMA na CCM na kwa maoni yao walisema si ajenda yao ya sasa, lakini Kamati Kuu baada ya ushawishi wakakubali.

“Kimsingi Katiba hatukatai lakini wenzetu wanataka Katiba ipatikane leo, katika kile kikao walituambia tunaelewa Katiba hii haitakuwa leo lakini tunawasihi mkubali uwepo wa Katiba, tukatoa tamko na muda mwafaka tutakubaliana.

“Wenzetu wanasema wanataka Katiba sasa, katika mkutano uliofanyika ukumbi wa Mwalimu Nyerere jijini Dar es Salaam Rais alisema Katiba mpya haiwezi kuwa ya vyama vya siasa peke yao,”amesema.

Ameongeza Katiba ya sasa imefanyiwa marekebisho mara 14 na sababu ukiangalia sio mambo yaliyohusu wananchi bali ni Siasa, madaraka na uchaguzi.








Wizara ya Elimu,Sayansi na Teknolojia kupitia Taasisi ya Elimu Tanzania(TET) inaendelea na kazi ya utoaji mafunzo kwa Walimu Wakuu wa shule za msingi za Serikali na zisizo za Serikali nchini kwa lengo la kuwajengea uelewa wa namna bora ya kusimamia na kufuatilia utekelezaji wa Mtaala wa Elimu ya Awali na Msingi wa Mwaka 2023.

Akizungumzia kuhusu mafunzo Mkurugenzi Mkuu wa TET , Dkt. Aneth Komba amesema kuwa mafunzo hayo yatafanyika Kwa walimu Wakuu wote katika Halmashauri 184 kuanzia leo tarehe 5/5/2024 hadi 12/6/2024 kwa awamu tofauti ambapo katika awamu ya kwanza, mafunzo yatafanyika katika Halmshauri za Mkoa wa Mwanza, Mara, Simiyu, Shinyanga, Kagera Kigoma, Geita na Tabora.

“Tunaendelea na mafunzo na awamu hii ni ya walimu wakuu wote nchi nzima ambapo tufanafaya mafunzo kwa awamu tofauti tofauti”amesema Dkt.Komba.

Aidha, Dkt. Komba ameeleza kuwa mafunzo ni ya muhimu kwakuwa walimu Wakuu wataweza kusimamia na kufuatilia utekelezaji wake na kuweza kutoa msaada (Mentorship and Support) kwa walimu wengine masomo pale inapohitajika.

Wawezeshaji na waratibu wa mafunzo hayo ni kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, OR-TAMISEMI na TET,huku akiishukuru Serikali ya Awamu ya sita inayoongzwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuwezesha mafunzo hayo kufanyika kwa walimu wote nchini.







Na Albano Midelo,Songea

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera,Bunge na Uratibu Mheshimiwa Jenista Mhagama amezindua mradi wa kuendeleza lishe na ufugaji endelevu wa viumbe maji kwa wakulima wadogo (ARSNA) unaogharimu shilingi bilioni 3.1 katika Kijiji cha Mpitimbi wilayani Songea mkoani Ruvuma.

Waziri Mhagama amesema mradi huo unaotekelezwa na serikali katika mikoa ya Ruvuma na Lindi kwa unafadhiliwa na serikali ya Norway kupitia Shirika la NORAD na kwamba unatekelezwa kwa kipindi cha miaka miwili kuanzia Machi 2024 hadi Machi 2026.

Ameutaja mradi huo kuwa umelenga kuleta mabadiliko makubwa kwenye uzalishaji na uendelezaji wa biashara ya ufugaji Samaki na uzalishaji wa mwani kwa lengo la kuwawezesha wananchi kunufaika katika maeneo yao ufugaji Samaki na uzalishaji wa mwani.

Amesema serikali imekusudia kuendeleza kilimo na uvuvi katika mikoa ya Ruvuma,Lindi ili kupata mafanikio makubwa na kuongeza tija na kukabiliana na changamoto kubwa ya upatikanaji wa vifaranga vyenye ubora na chakula cha Samaki.

“Kupitia mradi huu wazalishaji binafsi wa vifaranga vya samaki watajengewa uwezo katika uzalishaji wa vifaranga na wafugaji wa Samaki hususan vijana watajengewa uwezo wa kutengeneza chakula cha Samaki ’’,alisisitiza Mhagama.

Waziri Mhagama amesema tayari serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi imejenga shamba darasa la ufugaji wa samaki katika Kijiji cha Mpitimbi ambalo amesema litakuwa chachu kubwa katika ufugaji bora wa Samaki ambapo amewaomba wananchi hao kutumia shamba darasa hilo ili kuongeza tija katika ufugaji wa Samaki.

Ametoa rai kwa wakuu wa mikoa ya Ruvuma na Lindi ambako mradi huo unakwenda kutekelezwa kuhakikisha mradi unakwenda kutekelezwa kwa ufanisi mkubwa ili kupata tija na thamani halisi ya fedha zitakazotumika.

Awali akitoa taarifa ya mradi huo Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Sera,Bunge na Uratibu Underson Mutatembwa ameutaja mradi wa ARSNA kuwa unataarajia kuzifikia kaya 5,000 za wakulima wadogo ikijumuisha wanawake asilimia 50 vijana asilimia 40 na makundi mengine asilimia 10.

Amesema mradi huo unaogharimu shilingi bilioni 3.1 unatekelezwa katika kipindi cha miaka miwili kuanzia Machi 2024 hadi Machi 2026 katika Halmashauri za Wilaya ya Songea na Mbinga mkoani Ruvuma na Halmashauri za Wilaya za Mtama na Ruangwa mkoani Lindi .

Amesema Tanzania imekuwa moja ya nchi tatu za Afrika zilizopata fursa ya kunufaika na utekelezaji wa mradi huu nchi nyingine amezitaja kuwa ni Msumbiji na Kenya na kwamba mradi huo ni sehemu ya utekelezaji wa program kubwa ya kuendeleza kilimo na uvuvi inayofadhiliwa na Shirika la IFAD inayotekelezwa katika mikoa 12 ya Tanzania kwa gharama ya shilingi bilioni 150.

Akizungumza kwenye uzinduzi huo Mwakilishi wa Mkurugenzi IFAD Afrika Mashariki na Kusini Jacquiline Machangu amesema IFAD imekuwa ikifanya kazi na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ikiwemo sekta ya kilimo hususan wakulima wadogo waliopo vijijini.

Amesema IFAD kupitia mradi wa ARSNA imelenga kuongeza mapato na kujenga uwezo kimaisha wafugaji wadogo katika maeneo matatu.

Ameyataja maeneo hayo kuwa ni ongezeko la uzalishaji na ustahimilivu kwa wafugaji wadogo wa Samaki,kuongeza kwa fursa kwa wanawake na vijana kupitia ubunifu kwenye masoko na kuendeleza ujuzi na uundaji wa sera mpya.

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mheshimiwa Alexander Mnyeti akizungumza kwenye uzinduzi huo amesema Wizara hiyo itaendelea kutoa watalaam wa uvuvi ili kufanikisha mradi huo unakwenda kuzalisha Samaki wengi kwenye mabwawa ambao wana virutubisho muhimu.

Amesema Samaki wa mabwawa wanaweza kumaliza changamoto ya udumavu kwenye Mkoa wa Ruvuma ambapo hivi sasa udumavu umefikia asilimia 37 katika Mkoa wa Ruvuma , licha ya Mkoa huo kutajwa kuwa ni ghala la chakula nchini.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Ahmed Abbas Ahmed ameishukuru serikali kwa kuanza kutekeleza mradi huo mkubwa wa ufugaji Samaki katika Kijiji cha Mpitimbi.

Hata hivyo amesema serikali imekuwa inatekeleza miradi mikubwa katika jimbo la Peramiho ukiwemo mradi wa ujenzi wa barabara ya lami nzito kutoka Likuyufusi hadi Mkenda mpakani mwa Tanzania na Msumbiji.

Amesema mradi huo upo mbioni kuanza kutekelezwa serikali imetenga shilingi bilioni 74 kuanza kujenga lami kilometa 60 na kwamba serikali imetoa mabilioni ya fedha kutekeleza miradi mbalimbali ya kimkakati mkoani Ruvuma.

Ameitaja baadhi ya miradi iliyotekelezwa kuwa ni ujenzi wa barabara ya lami nzito kilometa 66 kutoka Mbinga hadi Mbambabay kwa gharama ya shilingi bilioni 127,ujenzi wa bandari ya kimkakati ya Ndumbi kwa gharama ya Zaidi ya shilingi bilioni 12 na ukarabati wa uwanja wa ndege Songea kwa gharama ya shilingi bilioni 37.










Nyumba ya kuishi familia mbili za walimu wa shule ya msingi Tunduru Mchanganyiko iliyojengwa kwa fedha kutoka serikali kuu ambayo itawawezesha walimu kuishi karibu na eneo lao la kazi.
Mratibu elimu katika kata ya Mlingotimashariki wilayani Tunduru Erith Banga katikati, akimsikiliza Mwalimu Mkuu wa shule ya msingi Tunduru Mchanganyiko Sabila Lipukila kushoto,kuhusu ujenzi na uboreshaji wa miundombinu ya elimu katika shule hiyo yenye watoto zaidi ya 1,738 kati yao wanafunzi 43 ni wenye mahitaji maalum,kulia Mwalimu wa shule hiyo Ambilikile Mwandembo.
Mwalimu Mkuu wa shule ya msingi Tunduru Mchanganyiko wilayani Tunduru Sabina Lipukila akiongea na baadhi ya wanafunzi wa darasa la saba wa shule hiyo juu ya umuhimu wa kutunza miundombinu ya elimu inayojengwa katika shule hiyo baada ya serikali kutoa zaidi ya Sh.milioni 300.

Na Mwandishi maalum, Tunduru
SERIKALI imetoa kiasi cha Sh.milioni 302 ili kuboresha mazingira na miundombinu ya kufundishia na kujifunzia kwa wanafunzi na walimu katika shule ya msingi Tunduru Mchanganyiko wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma.

Mwalimu Mkuu wa shule hiyo Sabina Lupukila amesema,kati ya fedha hizo Sh.milioni 246 zimetoka serikali kuu na Sh.milioni 56 zimetolewa na Halmashauri ya wilaya Tunduru.

Lipukila alisema,Sh.milioni 80 zimetumika kujenga bweni,Sh.milioni 50 kujenga nyumba moja ya walimu ya familia mbili,Sh.milioni 60 kujenga uzio na Sh.milioni 56 kwa ajili ya matundu 32 ya vyoo.

Aidha alieleza kuwa,Sh.milioni 56 zilizotolewa na Halmashauri ya wilaya Tunduru, Sh.milioni 41 zimetumika kumaliza ujenzi wa miradi hiyo iliyoanzishwa na serikali kuu na Sh.milioni 15 kwa ajili ya kununua vifaa vya kufundishia na kujifunzia.

Alisema,bweni lina uwezo wa kuchukua watoto 80 na katika awamu ya kwanza litatumika kulala watoto wa kike wakati serikali ikiendelea na mchakato wa kujenga bweni lingine la watoto wa kiume.

Alisema, kwa sasa shule ya Tunduru Mchanganyiko ina wanafunzi 1,738 kati yao wanafunzi 43 ni wa elimu maalum kuanzia darasa la awali hadi la saba ambao wanatoka nyumbani na kwenda shule kila siku.

Lipukila alisema,ujenzi wa bweni hilo ni mpango wa serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Dkt Samia Suluhu Hassan wa kuwajali watoto wenye mahitaji maalum na kuboresha mazingira ya elimu ili kuhamasisha watoto kupenda kusoma na wazazi kupeleka watoto wao shule kwa ajili kupata haki yao ya msingi.

Alisema,serikali inatambua umuhimu wa kuwa na mazingira mazuri ya kusoma ili kuwawezesha watoto wenye mahitaji maalum kusoma bila vikwazo vyovyote kutokana na changamoto zao za kimaumbile.

Alisema, bweni hilo ni dawa itakayotibu watoto wote wenye mahitaji maalum waliopo katika wilaya ya Tunduru kutopenda kusoma na wengine kuacha shule kwani sasa kuna sehemu nzuri na rafiki itakayowawezesha kutimiza ndoto zao.

“watoto wenye ulemavu sio kwamba hawana ndoto,lakini changamoto kubwa imetokana na mazingira magumu kwa baadhi ya wazazi,natoa wito kwa wazazi na walezi wote wenye watoto wenye mahitaji maalum wawalete watoto wao kwenye shule hii”alisema.

Mratibu elimu kata ya Mlingoti Mashariki Erith Banda,ameishukuru serikali kujenga bweni la wanafunzi wenye mahitaji maalum na nyumba moja ya kuishi walimu.

Alisema,bweni hilo litamaliza adha kwa watoto wanaoishi mbali na shule kutumia muda mrefu kila siku kwenda kufuata masomo na kuepukana na changamoto mbalimbali za njiani.

Ambilikile Mwandembo anayefundisha watoto wenye ulamavu alisema,watoto hao wamegawanyika kwenye makundi matatu ambayo ni walemavu wa akili,ulemavu wa kusikia,mabubu,wenye uono hafifu na walemavu wa ngozi.

Alisema,watoto walemavu wanafundishika hivyo wazazi wachae tabia na kasumba ya kuwaficha watoto hao nyumbani,badala yake wawapeleke shule wakapate haki yao ya msingi.

Samia Shabani mwanafunzi wa darasa la saba alisema,bweni hilo ni muhimu sana kwa wenzao wenye ulemavu kwani sasa watapata muda mwingi wa kusoma kwa sababu wataishi shuleni.
Katika kupambana na udumavu mkoani Njombe, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Njombe imeendelea kufikisha ujumbe kwa jamii kwa namna mbalimbali na sasa ni zamu ya Bajaji kufikisha ujumbe huo kupitia Mabango.

Bwana Chrispin Kalinga kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Njombe amesema lengo la kuweka mabango hayo ni kufikisha ujumbe kwa jamii na Bajaji ni miongoni mwa chombo cha usafiri kinachotumiwa na watu wengi hivyo anaamini ujumbe huo utafika kwa jamii.

"Bajaji inatumiwa na makundi mbalimbali na rika tofuati tofauti na unafahamu hapa mjini Njombe na pale Makambako wananchi wanatumia sana usafiri wa Bajaji kwahiyo tunaamini kwa njia hii ujumbe utawafikia na adhma ya Mkuu wa Mkoa wa Njombe Anthony Mtaka ni kuona udumavu unaisha ndani ya mkoa wetu" amesema Kalinga.

Baadhi ya Madereva Bajaji mjini Njombe wamesema hatua ya Ofisi ya Mkuu wa Mkoa kuwashirikisha kupeleka ujumbe wa Lishe ni hatua nzuri kwani inaonesha serikali inatambua Bajaji ni moja ya sehemu inayohudumia watu wengi na itarahisisha ujumbe huo kufika kwa wananchi.

Kwasasa Kampeni ya Lishe mkoani Njombe inabebwa na kaulimbiu inayosema "Kujaza Tumbo Sio Lishe Jali Unachokula/ Unachomlisha" ikilenga kuhamasisha jamii kuzingatia lishe bora kutokana takwimu za matokeo ya awali ya utafiti wa hali ya afya nchini zilizotolewa na Ofisi ya Takwimu Nchini (NBS) 2022 kuonesha mkoa huo bado una changamoto ya udumavu kwa asilimia 50.4, huku mkoa wa Iringa ukiongoza kwa asilimia 56.9.




Mwandishi wa kitabu cha “And the Children Shall Lead Us”  Barry Childs (katikati) akionyesha nakala ya kitabu hicho katika  hafla ya uzinduzi iliyofanyika jijini Dar e salaam hivi karibuni,wengine kwenye picha kushoto ni Mratibu wa mradi wa Africa Bridge  Kelvin Ngonyani  kulia ni mwandishi mwenza wa kitabu hicho, Philip Whiteley.

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
SHIRIKA la kuhudumia watoto walio katika mazingira magumu Africa Bridge limeweza kuwasaidia watoto 7,700 katika kata sita na vijiji 37 katika mkoa wa Mbeya wilaya ya Rungwe kwa kuwasaidia na elimu, malazi na afya.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam wiki iliyopita kwenye uzinduzi wa kitabu cha “And the Children shall Lead Us” mtunzi wa kitabu hicho Barry Childs alisema kwamba alirudi Tanzania baada ya miaka 35 na kuumizwa na hali aliyoikuta ya watu wa maeneo ya vijijini na kuamua kuanzisha shirika hilo la kutoa msaada.

“watu ambao wengi nilikua nao katika Mkoa wa Arusha kati ya 1944 hadi 1962 nilikuta hali zao bado ni duni na wengine walikuwa wameshapoteza maisha kutokana na umasikini wa kutupwa na nikaamua kuandika kitabu hiki ili kuleta mtazamo chanya wa kuweza kusaidia watu wa vijini hasa watoto,” alisema.

Alisema, muundo unaotumiwa na shirika hilo la Africa Bridge ni aina mbili kwanza kushirikisha watoto wenyewe na wazazi na pia kushirikisha jamii husika kupitia kwenye kamati za vijiji ili kuweza kusaidia katika malezi ya watoto kuanzia shule, nyumbani na kwenye jamii kwa ujumla.

Childs aliongeza kwamba kupitia mradi huo watoto wanajifunza shughuli za ujasiriamali kama vile kufuga ngo’mbe, kukamua maziwa na kuuza na upandaji na ulimaji wa zao la parachichi kwa ajili ya biashara,

Aliongeza kwamba utunzi wa kitabu hicho na uanzishwaji wa mradi huo unatokana na tafiti iliyofanywa na Chuo Kikuu Texas nchini Marekani kupitia kituo chao cha Utafiti cha Ray Marshall na kusema mfumo unaotumiwa na mradi utaleta matokeo chanya nchini Tanzania.

Kwa upande wake , Mratibu wa mradi huo, Kelvin Ngonyani alisema kwamba kitabu hicho chenye simulizi la kusisimua na kinacholenga kuwatoa watoto kwenye umasikini na kuwapa maarifa ya kilimo endelevu, ujasiriamali na kuboresha maisha yao hasa maeneo ya vijijini.

Aliongeza kwamba mfumo wa kuwahudumia watoto ni kwa kupitia kamati familia na jamii kwa kiwashirikisha viongozi wa kata, mitaa na vijiji ili kuweza kuleta ufanisi katika kutoa msaada wenye matokeo chanya kwa mtoto kuanzia malazi na elimu yao.

Mmoja wa wanufaika wa mradi huo , kutoka Mbeya wilaya ya Rungwe ni Sara Mosses (22) ambaye kwa sasa anasoma Chuo cha Rungemba Mafinga na anachukua Stashada ya Maendeleo ya jamii ambaye alisema....mie ni mmoja wa wanaufaika na mradi huu kwa kusomeshwa kupitia zao la parachichi kuanzia shule ya msingi, sekondari na kwa sasa nachukua stashada ya Maendeleo ya jamii na nataka kurudi kuendelea kuhudumia jamii yangu hasa watoto ambao wako kwenye mazingira magumu hapa nchini,”

Mtunzi wa kitabu hiki kinachoitwa “And the Children Shall Lead Us” (Na Watoto Watatuongoza) Barry Childs, ambaye alikulia Tanzania na baadaye alikwenda kusoma Shahada ya Sayansi katika Saikolojia katika Chuo Kikuu cha KwaZulu-Natal Afrika kusini.

Childs alifanya kazi kwa miaka 17 katika kampuni ya Exxon na baadaye alikuwa Mkurugenzi wa Masomo katika Maabara ya Abbott. Baada ya miaka 35 akiwa nje ya nchi, Childs ameamua kurudi Tanzania ili kuendeleza ndoto yake ya kuwatoa watoto kwenye umaskini.


Sehemu ya kitabu chake inasema kwamba aliporudi nchini alikuta watu wakipambana na umasikini na athari za ugonjwa wa Ukimwi, hivyo aliamua kujipanga akiwa kwenye shirika la Abbot 2000 na kuanzisha mradi unaoitwa ‘Africa Bridge’ kusaidia watoto wa Kitanzania.

Kitabu hiki chenye kurasa 168 kimechapishwa kwa lengo la kushirikisha jamii kwa jumla juu ya mafanikio ya mradi wa Africa Bridge katika kuleta uzoefu katika utafiti ya kitaaluma na kuzidisha uelewa kwa jamii juu ya uwezo wake mkubwa wa kuwainua watoto walio hatarini zaidi kutoka kwenye umasikini.

Childs aliamua kuanzisha mradi wa Africa Bridge ili kuionyesha dunia namna bora ya kutumia rasiliamali zilizopo kama ardhi na kilimo ili kuweza kumwinua mtoto wa Kitanzania na jamii kwa jumla kuondokana na umasikini.

“And the Children Shall Lead Us” kinaelezea jinsi mradi wa Africa Bridge unavyofanya kazi, ulivyotokea na kutekelezwa, na yale yaliyofunzwa katika miaka 23 ya uendeshaji wake.

Childs, ambaye ni mwanzilishi wa Africa Bridge, aliishi miaka yake ya utotoni Tanzania na alimua kurudi baadaye kujitolea kusaidia nchi yake ya asili.

Kitabu hiki, kinachokusudiwa kuwa somo pendekezi katika Sayansi za Jamii, kinaelezea simulizi la kuvutia la mradi wa Africa Bridge, shirika la jamii la pekee, ambalo limeendeleza mfano wa kujitegemea unaokubalika wa kuinua jamii za watu wa vijijini Afrika kutoka katika umaskini uliopitiliza.

Mwanzilishi wake Bw Childs anaamini kwamba ili kubadilisha maisha ya watoto walio hatarini, mtiririko salama wa mapato ni muhimu kwa kuwaendeleza, kupata elimu, na kutoa fursa halisi za kuwawezesha kufikia malengo yao.

Africa Bridge ilianzisha vyama vya ushirika vya kilimo na kamati za watoto na za kuwainua wanawake wa vijijini kwa kuwawezesha kwa vitendo ili kuzalisha mapato endelevu huku wakikidhi mahitaji ya jamii.


Mwanzilishi wa Mradi wa Africa Bridge na mtunzi wa Kitabu cha ‘And the Chidren Shall Lead Us, chenye simulizi ya kuwatoa watoto kwenye umasikini na kuwapa maarifa ya kilimo endelevu, kuboresha maisha yao, Barry Childs (katikati) akikata utepe kuzindua kitabu hicho kupitia mradi wa Africa Bridge nchini, hafla ya uzinduzi huo imefanyika jijini Dar es Salam.
Mwandishi wa kitabu cha “And the Children Shall Lead Us,  Barry Childs akielezea historia ya maisha yake nchini Tanzania na sababu ya kuandika  kitabu hicho.
Mwandishi wa kitabu cha “And the Children Shall Lead Us”  Barry Childs akibadilishana mawazo na Mwenyekiti wa Bodi wa mradi wa Africa Bridge nchini,Baraka Mtunga wakati wa hafla  hiyo.
Baadhi ya washiriki  wakifuatilia matukio mbalimbali wakati wa hafla hiyo.


Top News